KUPATIKANA kwa foda (fodder), na jinsi ya kuzihifadhi, ni miongoni mwa changamoto ambazo wakulima wengi huzipitia katika shughuli za ufugaji wa mifugo, hasa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.
Ili kuikabili changamoto ya jinsi ya kuhifadhi foda, wakulima wamebuni mbinu ya kuzihifadhi, kwa kuitumia mifuko ya plastiki, miongoni mwa mbinu nyinginezo.
Hata hivyo, mbinu hiyo imekuwa na changamoto, kwa sababu husababisha hewa ya oksijeni kutoa unyevu unaofanya kuvu kuota kwa lishe, na hivyo kufanya lishe kupoteza virutubisho muhimu na hata kuwa hatari kwa mifugo.
Pia, mifuko hiyo ya plastiki huwavutia wadudu pamoja na wanyama kama vile panya, wanaovutiwa na harufu inayotolewa na lishe zilizohifadhiwa kwa mifuko hiyo.
Kwa madhumuni ya kuikabali changamoto hiyo, kampuni ijulikanayo kama Packaging Industries Limited, imeanza kuitengeneza mikoba maalumu ijulikanayo kama ‘Mama Silage Bags’ ambayo itawasaidia wakulima kuzihifadhi lishe ipasavyo.
Mikoba hiyo hutumiwa kuzihifadhi lishe za mifugo kwa muda mrefu na hivyo kumuondolea mkulima wasiwasi.
Kwa mujibu wa Bi Vaishali Malde, meneja wa mauzo katika kampuni hiyo, mikoba hiyo ni bora kwa sababu haifanyi oksijeni kuwa na unyevu, na hivyo basi, lishe haziharibiki.
“Huku puya (molasses) zikitakikana kutumika kama kichocheo cha kuharakisha mchakato wa uchachukaji (fermentation) kwa mifuko mingine ya plastiki, mifuko ya ‘Mama Silage Bags’ huhakikisha kwamba sukari iliyoko kwa foda inatumika kuwa kichocheo, na hivyo kupunguza gharama ya kununua puya,” anaeleza Vaishali.
Bi Vaishali anaongeza kuwa, mikoba iyo hiyo, huzihifadhi lishe kwa muda mrefu, pasi na kupoteza virutubisho.
Aidha, anadokeza kuwa wakulima waitumiayo mikoba hiyo huimarisha uzalishaji na kuboresha afya ya mifugo.
“Mifuko hii hudumu kwa muda mrefu, hutumika mara kwa mara, na huhifadhi kilo 600 za lishe na huuzwa kwa Sh2,000, ikilinganishwa na mifuko mieusi, ambayo huuzwa Sh800, na huhifadhi kilo 200 hadi 300 tu za lishe,” anaongeza Bi Vaishali.
Mwenyekiti wa Naari Dairy, Geoffrey Imathew, anasema kuwa tangu aitumie mikoba ya ‘Mama Silage Bags’, amepata manufaa mengi, miongoni mwayo yakiwa ni kupungua kwa gharama ya uzalishaji na muda wa kuzitengeneza lishe.
“Sinunui puya (molasses) tena, ambazo ni ghali, ambazo zingetumika kuhifadhi lishe. Pia, siwahitaji watu wengi wa kunisaidia kwa mchakato huo, kwa sababu watu wawili au watatu huhitajika tu,’’ adokeza mkulima huyo.
Imathew anaongeza kuwa jambo jingine kuu ambalo analiona kwa mikoba hiyo ni kwamba, lishe haziharibiki, na hazivamiwi na wadudu au wanyama mathalani panya. Aidha, anasema kuwa mikoba hiyo ina harufu aula kwa wanyama, hivyo kuwanya wawe na hamu kuu ya kula lishe zinazohifadhiwa kwayo.
Mfugaji wa ng’ombe wa maziwa katika Kaunti ya Meru, Jeremy Murithi, anasema kuwa ameyaona manufaa ya kuitumia mikoba ya ‘Mama Silage Bags’ ambapo anafichua kuwa hakuna lishe zinazoharibika maadamu mifugo hula zote, au endapo kuna uharibifu, ni kiduchu tu, ikilinganishwa na mbinu ya zamani ya kuzihifadhi lishe.
Mkulima yuyo huyo andokeza kuwa gharama ya uzalishaji imeshuka, ikilinganishwa na wakati alikuwa akiitumia mbinu ya zamani ya kuzihifadhi lishe za mifugo wake.
Bi Vaishali anadokeza kuwa mikoba hiyo ina rangi mbili; rangi nyeupe nje, na nyeusi ndani, na mikoba yenyewe hupanuka inapowekwa lishe, na hivyo kuzihifadhi lishe nyingi mno.
Mikoba iyo hiyo, imetengenezwa kwa lengo la kuwanufaisha wakulima wadogowadogo wa ng’ombe wa maziwa, walio na ng’ombe kuanzia mmoja hadi watano, na ambao ni wakulima asilimia 80 nchini Kenya.
Bi Vaishali anasema hii ni mbinu ya kipekee ambayo huwasaidia wakulima kuzihifadhi lishe, na kuimarisha uzalishaji wa maziwa.